Mwanamke mmoja mkaazi wa Kilifi aliyenusurika kifo katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya hiyo, amesimulia kilichojiri katika msitu huo ambao ndani yake zaidi ya wafuasi 400 wa mhubiri Paul Mackenzie waliangamia.
Bi Salama Masha, anasema haikuwa rahisi kwake kukabiliana na changamoto alizopitia.
Anaelezea “Kabla ya kuhamia msitu wa Shakahola kutoka Malindi, mhubiri mgeni Mzungu alialikwa kanisani na kuhubiri kuhusu ishara za nyakati za mwisho,”
Mwanamke huyo anakumbuka mhubiri huyo akiwaeleza kuwa ishara za nyakati za mwisho duniani zinakaribia, injili ambayo alifungamanisha na mistari ya Biblia na matukio ya kisasa.
“Wahubiri katika Kanisa la Good News International walikuwa wakinukuu mistari ya Biblia hadi tukaamini,” alisema Bi Masha, akiongeza kwamba alipojiunga na Kanisa la Good News International la Paul Mackenzie alikuwa ameolewa.
“Mimi na mume wangu tulikuwa wafuasi wa kanisa hilo. Tulipoagizwa tusitembelee hospitali wala kuwapeleka watoto wetu shuleni nilitii kwa sababu niliona maisha hayo kuwa rahisi. Watoto wangu waligeuka kuwa wasomaji wazuri wa Biblia na nilijiuliza kama wanaweza kusoma Biblia vizuri kwa nini niwapeleke shuleni,” akasema Bi Masha.
Wakiwa wafuasi waaminifu wa mafundisho ya Mackenzie, kanisa lilipofungwa na tangazo kutolewa waelekee jangwani, yaani msituni Shakahola, Masha na familia yake walikuwa wa kwanza kutii agizo hilo.
“Mume wangu alinifahamisha kuwa alikuwa amenunua ekari mbili za shamba kwa Sh2000 huku Shakahola na tunapaswa kuhamia huko kuanza maisha mapya kwa kuwa waumini kadhaa wa kanisa hilo pia walikuwa wakihama. Nilikubali kwa sababu nilifurahi kwamba mume wangu amepata kipande cha ardhi cha ekari mbili kwa bei nafuu.”
Akiwa mzaliwa wa eneo la Chakama, karibu na Shakahola, alifurahi kuwa walikuwa wanahamia karibu na nyumbani.
Mwaka wa 2020, walihamia Shakahola. Tofauti na wafuasi wengine waliosafirishwa kwa lori, Bi Masha na familia yake walikwenda kwa hiari yao. Alisema waliishi maisha ya furaha kwa miaka miwili, hata wakajitosa katika kilimo.
Alipohamia Shakahola, Bi Masha alikuwa na watoto wanne. Alipata mtoto wa tano akiwa ndani ya msitu na alijifungua peke yake ndani ya nyumba yake iliyojengwa kwa matope.
“Mambo yalianza kubadilika Januari 2023 tulipoagizwa tuanze kufunga na kufungua jioni. Tulifunga pamoja na watoto wangu,” alisema.
Mwezi mmoja baada ya agizo hilo, mnamo Februari, mkutano wa mwisho ndani ya msitu huo uliitwa na wahubiri, lakini Bi Masha hakuhudhuria.
“Jirani alikuja na kunijulisha kuwa walipewa maagizo wasinieleze yaliyojiri katika mkutano huo kwa kuwa mimi ni mzaliwa wa eneo hilo na ningewasaliti wafuasi wenzangu. Maagizo yalikuwa nianze kufunga pamoja na watoto wangu hadi tutakapolala (kufa),” alisema Bi Masha.
Waliohudhuria mkutano huo wa mwisho walimfahamisha Bi Masha kwamba uliongozwa na mhubiri mwanamke kutoka Tanzania. Wanakijiji pia waliagizwa kutotembeleana na kubaki katika nyumba zao.
Walihimizwa kulinda nyumba zao kwa kuzingira ua wa miiba.
“Nilifunga siku tatu, lakini nilipoona watoto wangu wakiteseka sikuweza kuvumilia. Nilimpigia simu mama yangu aliyekuwa akiishi karibu na Shakahola kuja kunichukua.
Siku chache baadaye, mume wangu ambaye wakati huo alikuwa amedhoofika sana alikuja kunichukua akiomba turudi tukamilishe mfungo ili tukutane na Yesu sisi sote,” alisema Bi Masha.
Alielezea ugumu wa maisha kama vile kutafuta kazi za mikono ili kulisha watoto wake, ulimlazimu kurudi msituni na kumfuata mumewe.
“Mara ya pili tulipofunga kwa siku saba, watoto wangu walikuwa wakilia na kuomba maji ya kunywa. Niliishiwa nguvu, nilijiuliza kwa nini tunakufa njaa huku nyumba yangu ikiwa na chakula. Sikuweza kuvumilia tena na nikamuomba mume wangu anirudishe kwa mama yangu.
“Alikubali japo aliendelea kusisitiza kuwa tukiondoka mstuni tutaenda motoni na watoto. Nilirudishwa nyumbani na kupewa talaka kwa mdomo, ambayo kwa lahaja yetu ya Kigiriama tunaiita Sindikwa,” Bi Masha alisema.
Bi Masha na watoto wake walinusurika kifo lakini aliedelea na masaibu ya kukosa makao kwani kila siku anahama kutokana na usalama wake.
“Siwezi kukaa katika sehemu moja kwa muda mrefu sana. Hii ndiyo sababu ilikuwa vigumu kwao kunifuatilia. Ninapokea vitisho, serikali ililazimika kuingilia kati na kuwapeleka watoto wangu wanne kwenye kituo cha uokoaji ambapo walipo. Mzaliwa wa mwisho ambaye ana mwaka mmoja ndiye niliye naye pekee.”
Bi Masha sasa anaomba makazi salama kutoka kwa serikali.
By Matanda Emmanuel