Marais wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanakutana leo hii mjini Arusha, Tanzania.Katika mkutano huo,marais hao wamepangwa kujadili msururu wa masuala yanayohusu wananchi katika maeneo mbalimbali. Baadhi ya maeneo yatakayozingatiwa sana ni kuhusu uchumi na kwa kiasi kikubwa ushirikiano baina ya mataifa.
Mkutano huo ni Mkutano wa 23 wa Kawaida ya wakuu wa Nchi za EAC.Kwa mujibu wa EAC, viongozi hao watajadili ripoti ya mazungumzo ya kuandikishwa kwa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia katika jumuiya hiyo.
Somalia imekuwa ikishinikiza kukubaliwa katika umoja wa mataifa kwa karibu muongo mmoja sasa. Ripoti ya uthibitishaji ilipitishwa na marais kutoka sehemu mbalimbali duniani, wakati wa Mkutano wa 21 wa Kilele cha Kawaida huko Bujumbura, Burundi, Februari 4, 2023.Pia watajadili kuhusu ripoti ya maendeleo ya Mchakato wa Nairobi unaoongozwa na EAC, kuhusu kurejesha amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mchakato huo unaongozwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta wa kenya.
Viongozi hao wa Afrika Mashariki pia wataangalia ripoti ya maendeleo ya Mifumo Endelevu ya Ufadhili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Pia watajadili ripoti ya maendeleo ya Mashauriano ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la EAC.
Rais William Ruto Alhamisi jioni aliwasili Arusha, Tanzania kwa mkutano wa Afrika Mashariki.Pia alihudhuria mkutano wa ngazi ya juu wa mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula ambao uliandaliwa na EAC.
Ruto amekuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya ufadhili na mabadiliko ya hali ya anga ili kusaidia nchi za kipato cha kati kupambana vyema na mzozo wa mazingira unaosababishwa pakubwa haswa na mataifa tajiri. Marais wengine wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja na mwenyeji Rais Samia Suluhu Hassan na Évariste Ndayishimiye wa Burundi, Salva Kiir wa Sudan Kusini miongoni mwa wengine.
By Neema Faith