Kilifi, Kenya – Miili mitano imefukuliwa kutoka makaburi sita ya kina kifupi katika kijiji cha Kwa Binzaro, Kaunti ya Kilifi, kufuatia agizo la Mahakama. Operesheni hiyo inafanywa na maafisa wa upelelezi kutoka Kitengo cha Mauaji cha DCI wakishirikiana na wataalamu mbalimbali.
Maafisa hao wamesema wanatarajia kufukua zaidi ya makaburi 20 yaliyoko katika kijiji na vichaka vya jirani. Tukio hili linarejesha kumbukumbu za mauaji ya Shakahola ambapo zaidi ya watu 450 waliuawa, ingawa safari hii makaburi yameenea katika maeneo tofauti, na kufanya uchunguzi kuwa mgumu zaidi.
Makaburi 27 Yatambuliwa
Hadi sasa, jumla ya makaburi 27 yametambuliwa, wengi wa waliokutwa wakiwa watoto. Operesheni inayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mauaji, Martin Nyaguto, na mtaalamu wa serikali, Dkt. Richard Njoroge, itashirikisha wachimbaji, wataalamu wa uchunguzi wa maiti na makachero hadi makaburi yote yafukuliwe.
- DNA Kubaini Utambulisho
Miili iliyopatikana itafanyiwa uchunguzi wa DNA ili kubaini ni ya nani na kusaidia kurahisisha urejeshaji kwa familia.
- Uhusiano na Kanisa la Mackenzie
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa vifo 11 vinahusishwa na dhehebu linaloaminika kuwa na uhusiano na Kanisa la Good News International linaloongozwa na Paul Mackenzie, ambaye kwa sasa yuko gerezani kutokana na kuhusishwa na moja ya majanga makubwa ya kidini katika historia ya Kenya.
Story By Joel Esabu