Nairobi, Jumatatu, Agosti 25, 2025 – Rais William Ruto ametangaza na kuitawaza tarehe 27 Agosti kuwa Siku ya Katiba, kumbukumbu ya siku ambayo katiba ya sasa ya Kenya ilizinduliwa mwaka 2010.
Akilihutubia taifa asubuhi ya leo, Rais Ruto alisema maadhimisho hayo yataashiria miaka 15 tangu Kenya ilipopiga hatua muhimu katika safari yake ya kidemokrasia. Kwa mujibu wa Rais, Katiba Dei itaadhimishwa kila mwaka.
Rais alitaja katiba ya sasa kuwa mojawapo ya sheria endelevu na zenye umuhimu mkubwa katika historia ya taifa, akisisitiza ulazima wa kulinda haki za kimsingi na uhuru.
“Wakenya yafaa wakumbuke siku hii kwani inatukumbusha kuwa ni wajibu wetu kulinda, kutunza, kuzingatia na kutekeleza Katiba,” alisema Rais Ruto.
Aidha, Rais aliongeza kuwa Wakenya wote – walioko ndani ya taifa na hata kwenye mabalozi nje ya nchi – watashiriki katika siku hiyo kwa kujikumbusha wajibu wao wa kuzingatia katiba kupitia midahalo ya kitaifa kuhusu uongozi, utawala wa kisheria na haki za kikatiba.
Hata hivyo, Rais Ruto alibainisha kuwa Katiba Dei haitakuwa siku ya mapumziko. Badala yake, aliagiza taasisi zote za serikali, ikiwemo shule, kuandaa na kushiriki shughuli maalum za kuhamasisha wananchi ili kuongeza ufahamu wao kuhusu yaliyomo ndani ya katiba.